Mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kuhusu Ulinzi wa Taarifa Binafsi unafanyika Kigali Rwanda

Oct. 17, 2024, 6:31 p.m. Mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kuhusu Ulinzi wa Taarifa Binafsi unafanyika Kigali Rwanda

Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinafanya Mkutano kuhusu Ulinzi wa Taarifa Binafsi wenye lengo la kubadilishana ujuzi wa ulinzi wa taarifa na uthibitishaji wa mfumo wa sera ya usimamiaji wa taarifa. Mkutano huo unafanyika katika hoteli ya Radisson Parking Inn jijini Kigali, nchini Rwanda.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Bw. Emmanuel Mkilia ameeleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuna usalama wa taarifa binafsi kwa kutunga sheria inayohusiana na Ulinzi wa Taarifa Binafsi, kuanzishwa kwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na kuwepo kwa Kituo cha Data cha Taifa. 

“Taasisi mbalimbali nchini Tanzania zimeanza kushirikiana kupitia Mfumo wa Jamii Exchange unaowezesha kubadilishana taarifa. Mfumo huo unatarajiwa kuimarisha biashara mtandaoni (e-commerce) na uchumi wa kidijitali, ambao unaendelea kuimarika nchini na hivyo kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi Tanzania”.

Pia Bw. Mkilia amesisitiza umuhimu wa kuwa na miundombinu ya kuaminika katika kushirikishana taarifa kati ya nchi na nchi.

“Ni lazima kuwe na uaminifu katika miundombinu ili kuruhusu utumaji wa taarifa kwa usawa na ubora unaolingana, hivyo kuimarisha ushirikiano katika ulinzi wa taarifa binafsi.”

Mkutano huo wa siku tatu (3) unaoendelea jijini Kigali umeanza tarehe 16 na utaisha tarehe 18/10/2024 unashirikisha nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Tume za Ulinzi wa Taarifa Binafsi zilizopo kwenye nchi hizo. Kwa upande wa Tanzania, PDPC inawakilishwa katika Mkutano huo na Mkurugenzi Mkuu wa PDPC Bw. Emmanuel Mkilia, Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo ya Teknolojia PDPC Dkt. Noe Nko pamoja na Mwanasheria wa PDPC Bw. Godfrey Assenga