PDPC KUSHIRIKIANA NA WADAU KUIMARISHA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

Nov. 14, 2024, 3:41 p.m. PDPC KUSHIRIKIANA NA WADAU KUIMARISHA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia amesema PDPC imejipanga kuimarisha Ulinzi wa Taarifa Binafsi Nchini kwa vitendo ikishirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Na 11 ya mwaka 2022.

Dkt. Mkilia amesema hayo Novemba 13, 2024 jijini DSM wakati wa Uzinduzi wa Mafunzo ya maalum ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa Mahakimu wakazi wafawidhi nchini ambapo amesema jukumu la PDPC ni kulinda Taarifa Nchini na wamejitolea kuweka mfumo thabiti na wa vitendo wa kulinda Taarifa hizo kwenye sekta zote nchini. 

Aidha Dkt. Mkilia amesema jukumu PDPC si tu kutekeleza miongozo bali pia kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Idara ya Mahakama, Sekta Binafsi na Asasi za Kirai ili kukuza utamaduni wa kufuata sheria na utendaji bora katika Ulinzi wa Taarifa.

“Mahakama ina wajibu wa kulinda Taarifa nchini,hasa katika enzi hii ya kidijitali, kesi zinazohusu uvujaji wa Taarifa Binafsi, ukiukaji wa haki ya faragha na matumizi mabaya ya Taarifa zinapokuwa nyingi, jukumu lako kama hakimu litakuwa muhimu katika kuhakikisha haki inatendeka”. amesema Dkt. Mkilia. 

Mafunzo haya ya siku mbili yanatolewa na PDPC kwa kushirikiana na Jamii Forum @jamiiforums yanalenga kukuza uelewa wa Dhana ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa Mahakimu wakazi wafawidhi Tanzania na kuwajengea uwezo wa kutafsiri kesi, kusuluhisha mizozo na kutoa mwongozo unaolingana na kanuni za haki na uwazi kwenye kesi za Uvunjifu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.