PDPC NA HILTON LAW GROUP WAKUTANA NA WAANDISHI WA HABARI DODOMA

Nov. 26, 2024, 3:12 a.m. PDPC NA HILTON LAW GROUP WAKUTANA NA WAANDISHI WA HABARI DODOMA

Kuelekea warsha ya kuongeza uelewa kuhusu dhana ya Ulinzi wa taarifa binafsi inayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 17 hadi 18 Disemba 2024, leo tarehe 25 Novemba 2024, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) na Hilton Law Group wamezungumza na waandishi wa habari kuhusu warsha hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) ACP. Emmanuel Mkilia ameeleza kuwa mafunzo hayo ya uelewa kuhusu dhana ya Ulinzi wa taarifa binafsi yanawalenga wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi katika taasisi mbalimbali, Maafisa wa ulinzi wa taarifa binafsi kwenye taasisi hizo (DPOs) pamoja na wadau wengine.

“Tume ya Ulinzi wa taarifa binafsi kwa kushirikiana na Hilton Law Group tumeandaa warsha hii ya siku mbili ni muhimu hasa tunapoelekea ukomo wa maelekezo ya Mhe. Rais kwa taasisi za umma na binafsi kujisajili na Tume kabla au ifikapo tarehe 31 Disemba 2024” Amesema ACP. Mkilia

“Mpaka sasa zaidi ya taasisi 700 zimeshajisajili na Tume hivyo tunao maafisa ulinzi wa taarifa binafsi zaidi ya 700 kwenye taasisi hizo, hivyo tumeandaa warsha hii ili kuwajengea uelewa wa utekelezaji wa majukumu yao na tunayoyategemea kutoka kwao ili kurahisisha usimamizi na utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa taarifa binafsi namba 11 ya mwaka 2022. Warsha hii itawahusu zaidi DPOs, wanasheria na wadau mbalimbali wanaohusika na ulinzi wa taarifa binafsi ili waielewe dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi, wajibu wao na wajibu wa PDPC,” amesema ACP. Emmanuel Mkilia, Mkurugenzi Mkuu PDPC.

Kwa upande wake, mwanasheria wa Hilton Law Group, amewataka wadau wa ulinzi wa taarifa binafsi kuhudhuria warsha hii ili kupata uelewa na kutekeleza vyema sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za taasisi zao.

"Sisi kama Hilton Group tumeona umuhimu wa kushirikiana na PDPC kutoa uelewa huu kwa wadau ikizingatiwa kuwa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi ni mpya nchini kwetu. Tunaendelea kusisitiza kuwa ni muhimu kushiriki warsha hii hasa kwa taasisi binafsi na za serikali, wananchi na wanasheria ambao tunashirikiana na Serikali kutafsiri na kusimamia utekelezaji wa sheria za nchi. Hii ni warsha muhimu sana itakayotupa mwanga ya tunachotakiwa kukifanya, PDPC ni nini na majukumu yake ni yapi” amesema Doroth Ndazi, Wakili wa Hilton Law Group.

Warsha hii ya siku mbili itafanyika kuanzia tarehe 17 na 18 Disemba 2024 Jijini Dar es salaam katika ukumbi wa Superdome Masaki na washiriki wanatakiwa wajisajili kupitia tovuti ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi www.pdpc.go.tz na kuhakikisha wanapata nafasi ya kushiriki warsha hii ukumbini au kwa njia ya mtandao (online).