TUZINGATIE KANUNI ZA DHANA YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

Nov. 29, 2024, 2:27 p.m. TUZINGATIE KANUNI ZA DHANA YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

Dhana ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, ni dhana muhimu wakati huu wa mabadiliko ya kidijitali duniani hivyo ili kuendana na kasi ya Maendeleo ya Teknolojia Duniani Viongozi wa kada mbalimbali nchini wameshauriwa kuzingatia kanuni za Dhana ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kila wanapokua kwenye majukumu yao ya kila siku ili kuleta matokeo chanya kwenye sekta ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi

Hayo yameelezwa leo Novemba 29, 2024 Kisiwani Zanzibar na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ACP. Emmanuel Mkilia wakati wa hafla ya Ufunguzi wa semina kuhusu Dhana ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa Makatibu Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo amesema kama msingi wa Demokrasia ni wajibu wa kila kiongozi kuhakikisha haki ya Faragha inazingatiwa katika majukumu yao ya kikazi.

“Kama msingi wa demokrasia katika nchi yetu, pia Ulinzi wa Taarifa Binafsi umebainishwa na kuahidiwa pia katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 kipengele cha 61 (b). Kwa ajili hiyo basi, ni wajibu na jukumu letu, kama viongozi na watumishi wa umma, kuhakikisha kuwa haki hii inaheshimiwa katika mamlaka zetu.” Amesema ACP Mkilia

Aidha ACP Mkilia akawataka Makatibu Wakuu hao kuitumia Fursa hii ya Mafunzo kujadiliana kwa kina kuhusu Dhana ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

“ Tunapokusanyika hapa leo, hii ni fursa ya kujifunza na kutathimini umuhimu wa dhana nzima ya ulinzi wa taarifa binafsi katika nchi yetu na maisha ya wananchi lakini pia ulinzi na usalama wa taarifa za Taifa letu katika enzi ambapo taarifa zetu zinakusanywa na kuchakatwa kwa urahisi.”
PDPC kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi – Zanzibar wameandaa Semina hii ya siku moja kwa Makatibu Wakuu wa SMZ kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu Dhana ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Nchini.