Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi andaeni Taarifa za Mara kwa Mara

July 12, 2024, 3:46 p.m. Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi andaeni Taarifa za Mara kwa Mara

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi - PDPC, Bw. Emmanuel Mkilia amewataka Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini kuwa na utaratibu wa kuandaa taarifa za utekelezaji wa majukumu yao kila baada miezi mitatu ili kudumisha usalama wa Taarifa Binafsi na kuboresha ufuatiliaji wa mifumo yao kwa ufanisi.

Bw.Mkilia ametoa rai hiyo jijini Arusha wakati akifunga mafunzo ya Maafisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi - DPOs kutoka taasisi zilizo chini ya Chama cha Mabenki Tanzania - TBA na Chama cha Watoa Huduma za Mitandao ya Simu Tanzania - TAMNOA ambapo amesema kupitia mafunzo hayo ya siku nne wameweza kujifunza mbinu na maarifa mapya katika ulinzi wa taarifa binafsi, hivyo ni muhimu wakaweka mkazo katika kuandaa taarifa zao za utekelezaji mara kwa mara.

“Kuandaa taarifa kwa usahihi na kwa wakati ni muhimu sana katika kudumisha usalama wa taarifa hizo na pia kuhakikisha kwamba mnaweza kufanya ufuatiliaji wa mifumo yenu kwa ufanisi. Kwa hiyo, niwasihi muanze mara moja kuandaa taarifa za kila baada ya miezi mitatu ya utekelezaji wenu kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa.”  Amesema Bw. Mkilia

Katika hatua nyinginie Bw. Mkilia akawataka maafisa hao kuwa mabalozi wazuri wa waendelee kujifunza mbinu za kulinda Taarifa Binafsi kwa faida ya taasisi zao na Taifa kwa ujumla. 
“Kumbukeni kwamba ulinzi wa taarifa ni jukumu la kila mmoja wetu na ni sehemu muhimu ya ujenzi wa imani na uaminifu kwa wateja wetu. Nawatakia kila la kheri katika safari yenu ya kulinda taarifa binafsi na ninatarajia kuona mchango wenu chanya katika kuhakikisha kuwa taasisi zetu za kifedha na za watoa huduma ya mawasiliano ya simu zinakuwa salama na za kuaminika kwa wateja wetu.”

Mafunzo haya yameandaliwa na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini kwa kushirikiana na TBA na TAMNOA kwalengo la kuwajengea uwezo maafisa hao kwenye sekta ya kulinda taarifa binafsi na kuhakikisha usalama wa mifumo hiyo ya taarifa kwakua taarifa Binafsi ni mali muhimu sana kwa taasisi za kifedha na watoa huduma za mawasiliano.