TOA TAARIFA ZAKO KULINGANA NA HUDUMA UNAYOIHITAJI

Aug. 8, 2024, 5:23 p.m. TOA TAARIFA ZAKO KULINGANA NA HUDUMA UNAYOIHITAJI

<meta charset="UTF-8">

Jamii yaaswa kuzingatia kutoa Taarifa zinazoendana na huduma wanayoihitaji kwa wakati huo ili kulinda Taarifa zao Binafsi.

Wito huo umetolewa jijini Mwanza na Bw. Innocent Mungy, Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) wakati akifanya mahojiano maalumu kwenye kipindi cha Full Bando kinachorushwa hewani na  kituo cha redio cha Afya FM ambapo amesema ili kulinda matumizi ya Taarifa zako Binafsi, unapaswa kuchuja na kuhakikisha unapoenda kupata huduma, unatoa taarifa zinazoendana na huduma hiyo na si vinginevyo.

“ Mfano unaenda kukata bima ya gari ila unaulizwa una wake wangapi una haki ya kuhoji, we unataka kujua wake zangu ni wangapi ili iweje? Akikwambia anataka kujua kama na yeye ana gari na anakata bima kampuni gani unamwambia hapana kama atahitaji bima atakuja yeye mwenyewe, mimi nimekuja kama mimi” amesema Bw. Mungy

Aidha Bw. Mungy pia ametoa wito kwa Taasisi na Ofisi zote za Umma na binafsi nchini zinazotumia madaftari ya wageni kuyahifadhi sehemu salama madaftari hayo kwakua yana Taarifa Binafsi za watu na zinapaswa kulindwa kisheria.

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi imeweka kambi ya siku nne jijini Mwanza ili kutoa elimu kwa umma kuhusu Dhana ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa kushirikiana na vyombo vya habari mbalimbali jijini hapo ikiwa ni sambamba na kuhamasisha Taasisi na Ofisi zote zinazochakata na kukusanya Taarifa nchini kuhakikisha wanajisajili kwenye Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kabla ya Disemba 31, 2024 kama Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu alivyoagiza wakati wa Uzinduzi wa Tume hiyo.