TUMIENI TEKNOLOJIA VIZURI KULINDA TAARIFA BINAFSI

Sept. 21, 2024, 1:11 p.m. TUMIENI TEKNOLOJIA VIZURI KULINDA TAARIFA BINAFSI

Taasisi nchini zimetakiwa kuzingatia matumizi ya teknolojia zinazowezesha kulinda taarifa ili kuhakikisha hakuna uvunjifu wa Sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi nchini.

Hayo yamesemwa kwenye warsha ya ulinzi wa taarifa iliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadili teknolojia zinazoweza kusaidia kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi kwenye taasisi nchini Tanzania wakati taasisi hizo zikianza kutekeleza sheria hiyo ya ulinzi wa taarifa binafsi ya mwaka 2022.

Akizungumza kwenye warsha hiyo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Tafiti za Ulinzi wa Taarifa na Teknolojia kutoka Tume ya Ulinzi wa taarifa binafsi (PDPC), Dkt. Noe Nnko amezitaka taasisi za umma na binafsi nchini kuhakikisha zinazingatia sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa kutumia teknolojia vizuri na kulinda taarifa hizo.

“Taasisi zote za umma na binafsi lazima zihakikishe zimejisajili na kupata cheti cha PDPC kabla ya Disemba, 2024 ili kutii maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuheshimu sheria kwani kutokufanya hivyo ni kosa”

“Pia Taasisi zote zingatieni matumizi bora ya teknolojia za ulinzi wa taarifa kwenye mifumo yenu ili kulinda taarifa  vizuri. Sisi PDPC jukumu letu ni kusimamia na kuhakikisha ulinzi wa taarifa hizo unazingatiwa” amesema Dkt. Nnko 

Warsha hiyo imeandaliwa na PDPC kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) na kampuni ya Thales kutoka Afrika ya kusini na imejumuisha wataalamu wa teknolojia na sheria kutoka kwenye Wizara, Mashirika ya kiserikali na taasisi za umma 25 nchini.