TUSHIRIKIANE NA PDPC KUIMARISHA USALAMA WA TAARIFA BINAFSI

July 11, 2024, 9:51 a.m. TUSHIRIKIANE NA PDPC KUIMARISHA USALAMA WA TAARIFA BINAFSI

Balozi Adadi Mohamed Rajabu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi PDPC ameitaka Jamii kupitia Taasisi mbalimbali nchini kushirikiana na Tume ya ulinzi wa Taarifa Binafsi ili kuimarisha viwango vya Usalama wa Taarifa.

Balozi Adadi ametoa wito huo jijini Arusha wakati wa Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo ya siku nne ya Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi kutoka Taasisi zilizo chini ya chama cha mabenki Tanzania - TBA na chama cha watoa huduma za Mitandao ya simu Tanzania - TAMNOA ambapo amesema ushirikiano huo utajenga mazingira salama kwa Taarifa Binafsi za watu nchini.

“Napenda pia kutoa wito kwa sekta zote husika kushirikiana kwa karibu na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ili kuhakikisha kwamba viwango vya usalama wa taarifa vinazingatiwa na kwamba tunajenga mazingira salama kwa taarifa za watu’.

Katika hatua nyingine Balozi Adadi akawataka maafisa hao kuzingatia mafunzo hayo yanayotolewa na wabobezi kwenye kada ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

“Ninapenda kuchukua fursa hii kuwahimiza nyote mnaoshiriki mafunzo haya kuzingatia kwa makini kila somo mtakalofundishwa na watoa mada wetu ambao wote nimeona ni wabobezi wa masuala ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Usalama wa taarifa za watu ni jukumu letu sote, na ni muhimu kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuhakikisha kwamba tunatekeleza majukumu yetu ipasavyo”.