DPIA NI MUHIMU KUIMARISHA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

July 11, 2025, 3:55 p.m. DPIA NI MUHIMU KUIMARISHA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

Leo Ijumaa tarehe 11/07/2025 Maafisa wa Ulinzi wa Taarifa (DPOs) kutoka taasisi za umma na binafsi wamepatiwa mafunzo ya kina kuhusu namna ya kufanya Tathmini ya Athari za Ulinzi wa Taarifa (DPIA) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usimamizi na ulinzi wa taarifa binafsi katika taasisi zao.

Mafunzo hayo ya siku tatu (3) yaliyoandaliwa na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) yamefanyika katika ukumbi wa hoteli ya Morena, Morogoro yakilenga kuwajengea uwezo maafisa ulinzi wa taarifa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi kwa mujibu wa sheria na kanuni za ulinzi wa taarifa binafsi nchini.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Bw. Nsaa-Iya Kihunrwa amesisitiza umuhimu wa DPIA kama nyenzo muhimu katika kutambua na kupunguza athari kabla ya kuanzishwa kwa mfumo au mradi unaohusisha uchakataji wa taarifa binafsi wakati wa utekelezaji wake.

“DPIA ni mchakato wa lazima kwa taasisi zote zinazochakata taarifa binafsi. Kwa kufanya tathmini hii mapema, tunalinda haki za msingi za watu kwenye taarifa zao binafsi na pia tunazuia madhara ya kisheria au ya kiutendaji kwa taasisi zetu,” alisema Bw. Kihunrwa.

Mafunzo haya ya siku tatu yamehitimishwa leo ambapo yalihusisha ufafanuzi wa kina juu ya majukumu ya maafisa ulinzi wa taarifa kwenye taasisi zao na washiriki walipata fursa ya kujadili visa halisi, kushiriki katika makundi ya kazi, na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa sheria na teknolojia ya habari kuhusu changamoto wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi.

Mafunzo haya yanatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uelewa na utekelezaji wa Sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi, sambamba na kuinua viwango vya ulinzi wa taarifa binafsi nchini.