DPO SIMAMIA USALAMA WA TAARIFA BINAFSI KWENYE TAASISI/KAMPUNI YAKO

July 9, 2025, 5:26 p.m. DPO SIMAMIA USALAMA WA TAARIFA BINAFSI KWENYE TAASISI/KAMPUNI YAKO

Maafisa ulinzi wa taarifa (DPOs) wametakiwa kuhakikisha wanasimamia ulinzi wa taarifa binafsi kwenye taasisi zao.

Hayo yamesemwa leo Jumatano tarehe 9/7/2025 na Bi. Asha Sinare, mwezeshaji wa mafunzo kwa maafisa ulinzi wa taarifa ikiwa ni siku ya kwanza ya mafunzo maalum ya siku tatu kwa maafisa hao kutoka taasisi za umma na binafsi.

“Afisa Ulinzi wa taarifa binafsi (DPO) unapaswa kuwa na maarifa juu ya usalama wa mtandao ili uelewe hatari zilizopo zinazoathiri ulinzi wa taarifa binafsi kwenye taasisi/kampuni yako. Shughuli zote za kampuni zinazotumia taarifa binafsi za watu, DPO lazima uzitambue na uhakikishe utekelezaji wake unazingatia ulinzi wa faragha za taarifa hizo” amesema Bi. Aisha Sinare

Mafunzo ya maafisa ulinzi wa taarifa ni moja ya njia ya PDPC kuhakikisha maafisa hao wanaelewa na kutekeleza majukumu yao ya ulinzi wa faragha za watu kwenye taarifa binafsi zilizopo kwenye taasisi/kampuni zao.

Ulinzi wa taarifa binafsi ni takwa la kisheria na Tume ya Ulinzi wa taarifa binafsi inalisimamia hilo kuhakikisha utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44 unafanyika kikamilifu.