DPOs WAIPONGEZA PDPC KWA KUWAJENGEA UWEZO KATIKA ULINZI WA TAARIFA

Dec. 4, 2025, 7:08 p.m. DPOs WAIPONGEZA PDPC KWA KUWAJENGEA UWEZO KATIKA ULINZI WA TAARIFA

Washiriki wa mafunzo maalum ya Maafisa Ulinzi wa Taarifa (DPOs) wameipongeza Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kwa kuandaa na kutoa mafunzo mahususi yanayolenga kuwaongezea uwezo kwenye utendaji wao hasa katika kusimamia na kulinda taarifa binafsi ndani ya taasisi zao.

Wamesema mafunzo hayo yamewajengea uelewa wa kina kuhusu matakwa ya sheria, mbinu za kutathmini athari, na namna ya kuhakikisha taarifa za wananchi zinalindwa ipasavyo katika mfumo wa kidigitali unaokua kwa kasi.

“Mafunzo haya binafsi yamenifungua macho kuhusu umuhimu wa kuwa na mifumo madhubuti ya ulinzi wa taarifa tulizonazo kwenye kampuni yetu, na yametupa weledi wa jinsi ya kusimamia mzunguko mzima wa taarifa kuanzia ukusanyaji hadi uhifadhi. Nawapongeza sana PDPC, utayari wao wa kutoa mafunzo ya mara kwa mara ni ishara ya kujitoa katika kuhakikisha taifa linakuwa na wataalamu wenye uwezo wa kutosha kulinda taarifa binafsi’’ amesema Bw. Enock Helongwa, DPO - Taasa Luxurious Lodges & Camps.

“Naishauri PDPC kuendeleza utaratibu huu wa utoaji wa mafunzo ili kuwafikia Maafisa Ulinzi wa Taarifa wengi zaidi kwa sababu ulinzi wa taarifa binafsi ni eneo linalohitaji uelewa mpana ndani ya taasisi zote, bila kujali ukubwa au aina ya huduma inayotolewa” amesema Bi. Margaret Mhina, DPO - C. Steinweg Bridge Tanzania Limited.

Mafunzo hayo ya siku tatu kwa Maafisa Ulinzi wa Taarifa (DPOs) yanalenga kuhakikisha kila taasisi nchini inakuwa na DPO mwenye ujuzi wa kutosha kutekeleza misingi ya ulinzi wa taarifa kwa kuzingatia haki, uwazi, usalama na uwajibikaji. Mafunzo yamekuwa endelevu ikiwa hii ni awamu ya tano ambapo zaidi ya DPOs 200 wameweza kushiriki hivyo kuongeza idadi ya wataalamu wanaobobea katika fani hiyo muhimu.