ELIMU YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA YAWAFIKIA PDPC

Nov. 24, 2025, 10:12 p.m. ELIMU YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA YAWAFIKIA PDPC

Afisa uelimishaji kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma Bw. Faustine Malecha leo Jumatatu tarehe 24 Novemba, 2025 ametoa elimu kwa watumishi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kuhusu umuhimu wa kuzuia na kuepuka vitendo vya rushwa katika maeneo ya kazi.

Katika mafunzo hayo, yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi za PDPC, zilizopo Dodoma, Bw. Malecha amesisitiza kuwa rushwa si tu inashusha ufanisi wa taasisi za umma, bali pia inaathiri uaminifu wa wananchi kwa Serikali na kuhatarisha maendeleo ya Taifa.

“PDPC ni taasisi muhimu inayosimamia utekelezaji wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi, inapaswa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuhakikisha kuwa maamuzi yote yanafanywa kwa uadilifu, uwazi na haki” amesema Bw. Malecha.

Bw. Malecha pia alitoa mwongozo wa namna watumishi wanaweza kutambua viashiria vya rushwa, jinsi ya kuripoti vitendo vinavyohisiwa kuwa ni vya rushwa, na umuhimu wa kujenga utamaduni wa kuwajibika katika kila hatua ya utoaji huduma.

PDPC ina jukumu la msingi la kulinda haki ya faragha ya wananchi kwa kuhakikisha taarifa zao binafsi zinakusanywa, kuhifadhiwa na kutumika kwa mujibu wa sheria hivyo kujenga jamii inayotumia teknolojia kwa usalama, uaminifu na kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.