JENGA UAMINIFU WA TAASISI YAKO KWA WADAU KWA KULINDA TAARIFA ZAO BINAFSI

Aug. 20, 2025, 8:57 p.m. JENGA UAMINIFU WA TAASISI YAKO KWA WADAU KWA KULINDA TAARIFA ZAO BINAFSI

Ikiwa ni siku ya kwanza ya awamu ya nne ya mafunzo maalum kwa Maafisa ulinzi wa Taarifa Binafsi kutoka kwenye taasisi za umma na binafsi nchini, maafisa hao wametakiwa kuhakikisha taarifa binafsi za wadau wa taasisi zao zinalindwa kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44.

Akitoa mafunzo hayo Bi. Hellen Achimpota leo tarehe 20 Agosti, 2025 mkoani Morogoro amesema ni muhimu kuzingatia ukusanyaji wa taarifa binafsi unafanywa kwa lengo maalum tu, na kuhakikisha kuwa taarifa hizo hazitumiki nje ya madhumuni yaliyokusudiwa. Kwa kufanya hivyo taasisi hizo zitakuwa zinazingatia misingi ya kisheria ya faragha na heshima kwa haki za watu binafsi.

"Katika dunia ya sasa inayotawaliwa na teknolojia na matumizi makubwa ya taarifa za watu, ni muhimu kwa maafisa wa ulinzi wa taarifa binafsi kuelewa wajibu wao wa kisheria na kiutumishi. Misingi ya ukusanyaji wa idadi ya taarifa kulingana na makusudi husika , usalama wa taarifa, uhifadhi sahihi na usiri ni nguzo kuu katika kulinda haki ya faragha ya mtu binafsi," alisema Bi. Hellen 

Katika mafunzo hayo, washiriki wamepata fursa ya kujadili mifano halisi ya changamoto wanazokutana nazo kazini na kushiriki katika mazoezi kwa vitendo yaliyowasaidia kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi watakaporudi katika taasisi zao.

Mafunzo haya yanatarajiwa kuwa chachu ya maboresho katika usimamizi wa taarifa binafsi ndani ya taasisi mbalimbali, sambamba na utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini.

Tanzania Census 2022