MISHAHARA KWA WAFANYAKAZI NCHINI KUONGEZEKA JULAI, 2025

May 1, 2025, 8:49 p.m. MISHAHARA KWA WAFANYAKAZI NCHINI KUONGEZEKA JULAI, 2025

Watumishi wa umma nchini Tanzania leo tarehe 01/05/2025 wamepewa habari njema ya kuwepo kwa nyongeza ya mshahara kuanzia mwezi Julai, 2025.

Hayo ameyasema Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya wafanyakazi duniani iliyoadhimishwa mkoani Singida Kitaifa hapa Tanzania.

“Ninayofuraha ya kuwatangazia kwamba, katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi, mwaka huu Serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1. Nyongeza hii itaanza kutumika mwezi Julai 2025 itaongeza kima cha chini cha mshahara kutoka Tsh. 370,000 hadi Tsh. 500,000”  amesema Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Pia Mhe. Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Serikali inaendelea kusimamia upatikanaji wa ajira ndani na nje ya Tanzania.

“Jumla ya ajira 8,088,204 zimepatikana kwa kipindi cha Novemba, 2020 hadi Februari, 2025. Ukuaji wa diplomasia ya Tanzania imewezesha ipatikanaji wa fursa za ajira nje ya nchi.”

Hii ni moja ya hatua ambazo serikali inachukua kuwezesha watumishi kustahimili hali ya kiuchumi iliyopo

Maadhimisho hayo ni sehemu ya wafanyakazi kuwasilisha changamoto zao kwa Serikali na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kuboresha sekta ya ajira nchini. Kwa mwaka 2025 kauli mbiu yake ni Uchaguzi mkuu 2025 utuletee viongozi wanaojali haki na maslahi ya wafanyakazi, sote tushiriki.