MSINGI WA UCHUMI WA KIDIJITALI UNATEGEMEA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

Feb. 1, 2025, 12:20 a.m. MSINGI WA UCHUMI WA KIDIJITALI UNATEGEMEA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) Dkt. Emmanuel Lameck Mkilia amezungumza  katika mkutano wa GovStack, jijini Dar es Salaam na kusisitiza umuhimu wa kulinda faragha wakati mifumo inapoingiliana na kusomana

Mkutano huo uliofanyika kwa siku mbili na kufikia tamati leo uliandaliwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na jitihada ya GovStack kutoka nchini Estonia na uliangazia mifumo ya afya ya kidigitali, ambapo Dkt. Mkilia ameelezea majukumu ya PDPC katika kuhakikisha faragha inazingatiwa, hasa katika nyanja za afya katika dunia ya kidijitali. 

Aidha, Dkt. Mkilia alitaja hatua zinazochukuliwa ili kulinda taarifa binafsi za kiafya na umuhimu wa kuaminika ili watu waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali bila hofu. 

“Msingi wa uchumi huu wa kidijitali unategemea ulinzi wa taarifa binafsi na faragha.” Amesema Dkt. Mkilia

Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI, hospitali za serikali na binafsi kutoka Tanzania bara na Zanzibar.