NI KOSA KUSAMBAZA TAARIFA ZA MTU KWENYE MITANDAO YA KIJAMII BILA RIDHAA YAKE

Aug. 20, 2025, 8:58 p.m. NI KOSA KUSAMBAZA TAARIFA ZA MTU KWENYE MITANDAO YA KIJAMII BILA RIDHAA YAKE

Jamii yakumbushwa kutokusambaza au kutumia taarifa za mtu bila ridhaa ya mwenye taarifa.

Ushauri huo wa kisheria umetolewa leo Agosti 20, 2025 na Wakili Godfrey Assenga, Mwanasheria wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) wakati akijibu swali la mmoja wa washiriki wa Mafunzo Maalumu ya Maafisa Ulinzi wa Taarifa (DPO's) yanayoendelea hapa Morena Hoteli Mkoani Morogoro, ambapo aliulizwa je wale wanaosamba taarifa za watu kwenye makundi sogozi (WhatsApp groups) bila kuwa na ridhaa ya wahusika wa taarifa hizo nao wanavunja Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44 (PDPA)?

Akijibu swali hilo Wakili Asenga amesema, ndio ni kosa kisheria kwa mujibu wa Kanuni za Ukusanyaji na Uchakataji wa Taarifa Binafsi za mwaka 2023 na akasisitiza hata wale wanaosamba taarifa za watu kupitia mitandao ya kijamii hawaruhusiwi kufanya hivyo kama hawajapata ridhaa ya muhusika wa taarifa.

"Kanuni ya 15 (1) ya Kanuni za ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi za mwaka 2023 inazungumza mhusika wa taarifa anaweza kuomba kwa mkusanyaji au mchakataji kusitisha ukusanyaji au uchakataji wa taarifa binafsi muda wowote hivyo muhusika wa taarifa akiomba ridhaa ya kufutwa kwa taarifa zake unapaswa kumsikiliza na kuzifuta na endapo ukikaidi ombi lake ana haki ya kuja kulalamika PDPC na Sheria itafata mkondo wake” Amesema Wakili Asenga

Aidha Wakili Asenga alihitimisha kujibu swali hilo kwa kunukuu msemo maarufu wa kutokujua Sheria sio kigezo cha kuvunja Sheria.

Tanzania Census 2022