PDPC TUNAHAKIKISHA ULINZI WA FARAGHA ZA WATU KWENYE TAARIFA ZAO BINAFSI

Feb. 6, 2025, 4:49 p.m. PDPC TUNAHAKIKISHA ULINZI WA FARAGHA ZA WATU KWENYE TAARIFA ZAO BINAFSI

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) ipo kwa ajili ya kusimamia ulinzi wa faragha za watu hasa kwenye taarifa zao binafsi.

Hayo ameyasema leo, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC Dkt. Emmanuel Mkilia akimkaribisha Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa alipotembelea banda la PDPC kwenye maonesho wa wiki ya anwani za makazi yanayofanyika katika viwanja vya ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete uliopo Dodoma ambapo Mhe. Silaa alifungua maadhimisho hayo.

Dkt. Mkilia ameeleza kuwa anwani ya makazi ni moja ya taarifa binafsi za mtu ambayo isipotumika vyema inaweza kuleta madhara kwa muhusika wa taarifa.

“Anwani ya makazi ni moja ya taarifa binafsi na ni muhimu ijulikane pale tu panapokuwa na ridhaa ya muhusika wa taarifa hiyo anapotaka kupata huduma. PDPC tunasimamia ulinzi wa taarifa binafsi kwa kuhakikisha wakusanyaji na wachakataji wa taarifa hizo wanazingatia faragha pale wanapozitumia.”

Akifungua maadhimisho hayo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa ameeleza kuwa uwepo wa anwani ya makazi unarahisisha utoaji wa huduma mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii hasa zama hizi za mapinduzi ya viwanda yanayotegemea matumizi ya TEHAMA ambayo yanalazimu kuwa na mifumo ya utambuzi.

PDPC wameshiriki kwenye maadhimisho hayo ya wiki ya anwani ya makazi ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini, na yamefunguliwa rasmi leo tarehe 06/02/2024 jijini Dodoma yakiwa na kauli mbiu inayosema “Tambua na Tumia Anwani za makazi kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma.”