PDPC YATOA WITO WA USAJILI WA TAASISI ZA UMMA NA BINAFSI KABLA YA SIKU YA UKOMO 30 APRILI 2025

April 30, 2025, 10:20 p.m. PDPC YATOA WITO WA USAJILI WA TAASISI ZA UMMA NA BINAFSI KABLA YA SIKU YA UKOMO 30 APRILI 2025

Wakati dunia ikisherehekea maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imetahadharisha kuwa taasisi zote za umma na binafsi nchini zinapaswa kuwa zimesajiliwa rasmi kabla ya tarehe 30 Aprili 2025. Hii ni baada ya ukomo wa awali wa usajili ulioelezwa kuisha tarehe 31 Desemba mwaka jana, ambapo zoezi la usajili liliongezwa kwa hiari.

Katika mjadala huo uliohudhuriwa na Taasisi za Serikali zinazoshughulikia masuala ya habari, teknolojia, na ulinzi wa faragha, Dkt. Mkilia alisisitiza kwamba sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi haikusudii kuzuia au kukwamisha sheria nyingine kama ile ya Haki ya Kupata Habari au Uhuru wa Vyombo vya Habari na Uhuru wa Kujieleza bali kuhakikisha faragha na taarifa binafsi zinalindwa.

“Sheria hii inalenga kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na haki ya wananchi kupata habari, huku ikihakikisha faragha ya watu inahifadhiwa. Wajibu wetu ni kuhakikisha kuwa taarifa binafsi za watu zinazingatiwa na zinalindwa kikamilifu,” alisisitiza Dkt. Mkilia.

Akiendelea kuzungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Dkt. Emmanuel Mkilia, amesema dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi pia ni muhimu kwa waandishi wa habari na wadau wa sekta hiyo, ikiwa ni sehemu ya kufuata sheria na kanuni za uandishi wa habari pamoja na sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi.

“Uandishi wa habari ni taaluma inayofuata misingi ya haki na ukweli, hivyo ni wajibu wa kila mwandishi kuzingatia matakwa ya sheria hizi ili kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari na haki ya wananchi kupata habari unafikiwa,” alisema Dkt. Mkilia.

Maadhimisho ya mwaka huu yana kwa kauli mbiu inayosisitiza mustakabali wa uhuru wa vyombo vya habari unaoambatana na uwajibikaji, huku ikilenga kuhimiza usalama wa haki za wanahabari na wananchi kwa ujumla, wakati huu wa ukuaji wa kasi wa Teknolojia na matumizi ya Akili Unde, ikisisitiza matumizi ya teknolojia na ubunifu katika kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Uandishi wa Kijasiri na Mustakabali wa Uhuru wa Vyombo vya Habari na Media wakati huu wa matumizi ya Akili Unde” Kauli mbiu hii inalenga kuhimiza uelewa na umuhimu wa teknolojia na ubunifu katika kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari, huku ikilenga pia kuimarisha uwajibikaji na ufanisi wa sekta hiyo.