RIDHAA INAPASWA KUTOLEWA BILA SHURUTI

June 24, 2025, 2 p.m. RIDHAA INAPASWA KUTOLEWA BILA SHURUTI

Wakusanyaji na wachakataji wa Taarifa Nchini wameshauriwa kukusanya na kuchakata Taarifa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Sura ya 44 (PDPA) ikiwa ni pamoja na kutowashurutisha wahusika wa Taarifa kuwapatia ridhaa.

Wito huo umetolewa jijini Arusha, leo Juni 24, 2025 na Wakili Humphrey Mtuy, Mkuu wa Kitengo cha Sheria,Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC). Wakati akitoa mada ya Masuala Muhimu ya Kisheria katika PDPA kwa washiriki wa  mafunzo ya kupunguza madhara ya vihatarishi katika Ulinzi wa Taarifa Binafsi ambapo amesema kwa mujibu wa PDPA hairuhisiwi kuchukua ridhaa ya Muhusika wa Taarifa kwa Shuruti.
“Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Kifungu cha Thelathini (30) kifungu kidogo cha Kwanza (1) na Kanuni ya Ishirini na Tano 25 (d) ya Ukusanyaji na Uchakataji wa Taarifa imeanisha mazingira ya kuchukua ridhaa kwa Muhusika wa Taarifa hivyo inapaswa kutoa ridhaa bila shuruti” Amesema Wakili Mtuy

Aidha wakili Mtuy alikamilisha mada yake kwa kusema kwamba PDPA imekuja kumlinda muhusika wa Taarifa na imeruhusu PDPC kushirikiana na vyombo vingine vya dola kumpatia haki ya Faragha Muhusika wa Taarifa endapo Taarifa zake zikitumika vibaya.