π“π€π€π’πˆπ’πˆ π™πŽπ“π„ ππ‚π‡πˆππˆ 𝐍𝐈 π‹π€π™πˆπŒπ€ πŠπ”π–π€ 𝐍𝐀 π€π…πˆπ’π€ π”π‹πˆππ™πˆ 𝐖𝐀 π“π€π€π‘πˆπ…π€

Feb. 11, 2026, 2 p.m. π“π€π€π’πˆπ’πˆ π™πŽπ“π„ ππ‚π‡πˆππˆ 𝐍𝐈 π‹π€π™πˆπŒπ€ πŠπ”π–π€ 𝐍𝐀 π€π…πˆπ’π€ π”π‹πˆππ™πˆ 𝐖𝐀 π“π€π€π‘πˆπ…π€

Taasisi zote za umma na binafsi nchini zimetakiwa kuhakikisha zinakuwa na maafisa ulinzi wa taarifa (DPOs) ili kurahisisha utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Sura ya 44.

Hayo yamesemwa leo Februari 11, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Benno Malisa wakati akifungua mafunzo maalum kwa Maafisa Ulinzi wa Taarifa (DPOs) kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyoandaliwa na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na kufanyika katika ukumbi wa City Park Garden jijini Mbeya.

β€œTaasisi zote ambazo hazina maafisa ulinzi wa taarifa binafsi ziharakishe kuweka maafisa hao ili kutekeleza matakwa ya kisheria. Utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Sura ya 44 uendane na adhabu kwa watakaovunja sheria hiyo”

β€œKutokana na umuhimu wa kulinda faragha za watu nchini, mafunzo haya ni fursa ya kuweka utaratibu wa kuweza kuwapata maafisa ulinzi wa taarifa walio bora na hivyo kurahisisha utekelezaji wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi” amesema Mhe. Malisa.

Mhe. Malisa pia amewaomba PDPC licha ya kuwa na jukumu kubwa la kutoa elimu na kuhamasisha hizi taasisi kujisajiri PDPC kwa mujibu wa sheria, ni vizuri PDPC iwe na utaratibu wa kukutana na DPOs mara kwa mara kwa lengo la kuwaongezea ujuzi juu ya dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi.

Kwa umuhimu wa mafunzo hayo, Mhe. Malisa amewataka wanaopatiwa elimu hiyo kuifanyia kazi mara baada ya mafunzo ili kusaidia jamii kufahamu haki na wajibu wao wa kulinda taarifa zao pia kusaidia taasisi zao kuwa na misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi wanazozitumia.

Mafunzo hayo maalum kwa maafisa ulinzi wa taarifa yameanza leo Februari 11, 2026 ikiwa ni awamu ya Saba ya mafunzo ya namna hiyo na kwa awamu hii yanafanyika jijini Mbeya kwenye ukumbi wa City Park Garden na yanatarajiwa kumalizika Februari 13, 2026.