ULINZI WA FARAGHA KWENYE TAARIFA BINAFSI UNAJENGA IMANI YA WANANCHI KWA TAASISI

Sept. 11, 2025, 11:23 a.m. ULINZI WA FARAGHA KWENYE TAARIFA BINAFSI UNAJENGA IMANI YA WANANCHI KWA TAASISI

Mkurugenzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Ofisi ya Zanzibar Bi. Rehema Abdalla ameukumbusha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF) kuendelea kutunza faragha za taarifa za wateja wao kwa kuhakikisha wanatumia  taarifa wanazozikusanya au kuzichakata kwa misingi inayokusudiwa tu.

Bi. Rehema ameyasema hayo katika mafunzo ya siku moja kwa watumishi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Ofisi ya Zanzibar yaliyotolea na Afisa wa PSSSF Bw. Seif Khamis yakilenga kuwajengea uelewa watumishi hao juu ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma.

“Ninausifu Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma kwa kutumia teknolojia mpya inayorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja. Nawasihi katika utekelezaji wa shughuli zenu kuzingatia faragha katika kukusanya na kuchakata taarifa za wateja wenu ili kujenga imani kwa  wanachama wa mfuko huo” amesema Bi. Rehema

Msisitizo wa ulinzi wa  faragha za taarifa za watu ni njia mojawapo ya kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kuhakikisha taasisi zote za umma na binafsi zinazingatia kanuni za ulinzi wa faragha, ili kujenga imani ya wananchi katika mifumo ya kidigitali.

Tanzania Census 2022