WATENGENEZA MAUDHUI MWANZA WAKUMBUSHWA UMUHIMU WA KULINDA TAARIFA BINAFSI MTANDAONI

April 1, 2026, 10:28 p.m. WATENGENEZA MAUDHUI MWANZA WAKUMBUSHWA UMUHIMU WA KULINDA TAARIFA BINAFSI MTANDAONI

Watengeneza maudhui ya mtandaoni jijini Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla wamehimizwa kuzingatia dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi kama sehemu muhimu ya uwajibikaji wao katika enzi hizi za kidijitali ili kulinda faragha za watumiaji na kujenga uaminifu kwa jamii.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) Bw. Innocent Mungy wakati akiwasilisha mada jijini Mwanza kuhusu umuhimu wa ulinzi wa taarifa binafsi kwa watengeneza maudhui ambapo amesisitiza kuwa wao wanabeba jukumu kubwa si tu la kuburudisha bali pia kulinda taarifa za watu wanaowahusisha katika maudhui yao.

“Watengeneza maudhui mnahusika moja kwa moja katika ukusanyaji, uchakataji na usambazaji wa taarifa binafsi kupitia shughuli zenu za kila siku, hivyo mnapaswa kuzingatia ridhaa ya wahusika na kutumia taarifa zao kwa madhumuni yaliyokusudiwa tu kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44” amesema Bw. Mungy.

Bw. Mungy pia alifafanua kuwa taarifa binafsi ni pamoja na majina, namba za simu, picha, maeneo ya watu na hata taarifa za kifedha, na kusisitiza kuwa kutokuzilinda kunaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza uaminifu wa wafuasi, kuharibu taswira na hata kukumbana na hatua za kisheria.

Jukwaa hilo pia limetumika kuwakumbusha watengeneza maudhui kuhakikisha wanajisajili PDPC kabla ya mwisho wa kipindi cha usajili wa hiyari kinachotarajiwa kufungwa tarehe 8 Aprili 2026, ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na kutokuzingatia matakwa hayo ya kisheria.