DKT. MKILIA AFUNGUA WARSHA JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA

March 1, 2025, 2:16 p.m. DKT. MKILIA AFUNGUA WARSHA JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa taarifa binafsi (PDPC) Dkt. Emmanuel Mkilia, leo Jumamosi tarehe 01/03/2025 amefungua rasmi warsha ya dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa Jukwaa la wahariri wa vyombo vya habari nchini (TEF)

Akifungua warsha hiyo, Dkt. Mkilia ameeleza kuwa vyombo vya habari vina wajibu mkubwa katika ulinzi wa faragha za watu nchini.

“Katika suala hili tumeona umuhimu wa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari na kuhakikisha kuwa taarifa binafsi za watu haziwekwi hadharani bila ridhaa yao au bila uhalali wa kisheria hususani sheria zinazosimamia Sekta ya Habari na Mawasiliano nchini huku ukizingatiwa umuhimu wa haki za wananchi kupata habari.”

“Jukwaa la Wahariri ni wadau wakubwa wa PDPC kwa kuwa ni moja ya wachakataji wa taarifa. Ni daraja kati ya wakusanyaji wa taarifa (waandishi au watangazaji wa habari) na walaji wa taarifa hizo (wasikilizaji au wasomaji)” amesema Dkt. Mkilia

PDPC imesimama kati ya teknolojia na maisha ya watu, ipo kwa ajili ya kuhakikisha faragha za watu zinalindwa.  Teknolojia ni kwa ajili ya kuhakikisha na kurahisisha upatikanaji wa huduma  kwa wakati na kwa usahihi hivyo ni muhimu faragha zilindwe kwenye taarifa hizo ambayo ni moja ya haki za binadamu.

Warsha hiyo ya siku moja imefanyika katika ukumbi wa hoteli ya Morena iliyopo mkoani Morogoro. Hii ni moja ya njia ya PDPC kutoa uelewa wa dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa wadau wake mbalimbali.