ELIMU YA DHANA YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI YAWAFIKIA SHIVYAWATA

March 20, 2025, 11:44 p.m. ELIMU YA DHANA YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI YAWAFIKIA SHIVYAWATA

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) leo Alhamisi tarehe 20/03/2025 imetoa elimu ya dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa wanachama wa Shirika la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) kwenye kongamano la wanawake wenye uhitaji maalum lililofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ushirika mkoa wa Ruvuma.

Akizungumza katika kongamano hilo, Wakili Humphrey Mtuy, Mkuu wa Kitengo cha Sheria PDPC amewataka wanawake wenye uhitaji maalum  kuzingatia ulinzi wa taarifa zao binafsi pale wanapotakiwa kuzitoa ili wapatiwe huduma mbalimbali.

“Wanawake wenye uhitaji maalum mna changamoto mbalimbali zinazowafanya muwe na uhitaji wa huduma mbalimbali za kijamii. Upatikanaji wa huduma hizi unawalazimu mtoe taarifa mbalimbali zikiwemo taarifa zenu binafsi. Hivyo tunawafundisha sheria hii ya ulinzi wa taarifa binafsi ili mjue mna haki ya kujua kwa nini taarifa zenu zinachukuliwa na ni kwa namna gani zinakusanywa na kuchakatwa” amesema Wakili Mtuy.

Naye mratibu wa Shirika la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Bw. Suleiman Zalala ameishukuru Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa kuwapatia elimu hiyo kwa kuwa ni muhimu sana hasa kwa kundi la watu wenye uhutaji maalum.

“Tunawashukuru sana Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa kuridhia kutupatia elimu hii ya ulinzi wa taarifa binafsi. Kwa mara ya kwanza mmeshiriki kutupatia elimu watu wenye uhitaji maalum, hii ni hatua kubwa na mmeonyesha kututhamini sana” amesema Bw. Zalala.

Utoaji wa elimu kwa umma juu ya dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi ni kazi endelevu ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ili kuhakikisha jamii ambao ndiyo wahusika wakuu wa taarifa hizo binafsi wanafahamu umuhimu wa kulinda taarifa zao na kuhakikisha zinakusanywa na kuchakatwa kwa madhumuni maalum ili kujenga jamii inayozingatia ulinzi wa faragha hasa katika maendeleo ya kidijitali nchini na duniani kwa ujumla.