NI LAZIMA KUWA NA SERA YA ULINZI WA TAARIFA KWENYE TAASISI/KAMPUNI YAKO

July 10, 2025, 4:46 p.m. NI LAZIMA KUWA NA SERA YA ULINZI WA TAARIFA KWENYE TAASISI/KAMPUNI YAKO

Taasisi/kampuni zote za umma na binafsi zinazochakata na kukusanya taarifa binafsi zimetakiwa kuwa na Sera ya ulinzi wa taarifa ili kurahisisha uzingatiaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Kanuni zake wakati wa kutekeleze majukumu yao.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi tarehe 10/07/2025 na Mkurugenzi wa Tafiti za ulinzi wa taarifa na teknolojia Dkt. Noe Nnko kwenye mafunzo maalum kwa maafisa ulinzi wa taarifa (DPOs) kutoka kwenye taasisi za umma na binafsi nchini.

“Sera ya faragha na ulinzi wa taarifa inaeleza jinsi taasisi/kampuni inavyokusanya, kutumia, kushiriki na kulinda taarifa binafsi kulingana na muongozo wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44. Sera hii inatumika kwa wafanyakazi wote, wakandarasi, wadau na wahusika wengine ambao huchakata taarifa binafsi chini ya udhibiti wa taasisi/kampuni husika. Inajumuisha namna ya kushughulikia maombi ya taarifa husika, itifaki za majibu ya ukiukaji wa taarifa hizo, uainishaji na uhifadhi wa taarifa, idhini ya ukusanyaji na ufutaji wa taarifa, ukaguzi na ufuatiliaji” amesema Dkt. Noe Nnko.

“Sera hizi zinatofautiana kati ya taasisi moja na nyingine. DPO anatakiwa kutengeneza sera hiyo kulingana na asili ya taasisi/kampuni yake. DPO anapaswa kumsaidia mwajiri namna ya kulinda faragha ya taarifa binafsi, kusaidia kitengo cha Tehama jinsi ya kuzingatia ulinzi wa taarifa wakati wa kuandaa mifumo ya uendeshaji wa taasisi/kampuni yake.  Hivyo ni muhimu kuwasiliana na PDPC kwa swala lolote linalohusu ulinzi wa taarifa binafsi ili kupata msaada wa kitaalamu zaidi” amesema Dkt. Noe Nnko.

Mafunzo haya kwa maafisa ulinzi wa taarifa kutoka taasisi/kampuni za umma na binafsi yanafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 9 hadi 11/07/2025 yakilenga kuwajengea uwezo DPO juu ya utekelezaji wa majukumu yao katika kuimarisha uwezo wa utekelezaji bora wa mfumo wa kisheria wa ulinzi wa taarifa binafsi.