PDPC KUANZISHA ITHIBATI KWA MAAFISA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI NCHINI

July 16, 2025, 3:10 p.m. PDPC KUANZISHA ITHIBATI KWA MAAFISA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI NCHINI

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) ipo katika mpango wa kuwa na  Ithibati kwa Maafisa Ulinzi wa Taarifa (DPOs) ili kuhakikisha ulinzi wa taarifa binafsi nchini unazingatiwa.

Hatua hii inalenga kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi na kuhakikisha kuwa waliopewa jukumu la ulinzi wa faragha za taarifa hizo wanazingatia viwango vya juu vya ufanisi na uadilifu.

Hayo yamesemwa leo tarehe 16/07/2025 na Mkurugenzi Mkuu wa PDPC Dkt. Emmanuel Mkilia alipotembelea kituo cha mafunzo maalum ya maafisa ulinzi wa taarifa kilichopo kwenye hoteli ya Morena, Morogoro na kuzungumza na washiriki wa mafunzo hayo ambapo alisisitiza kuwa mafunzo hayo ni hatua muhimu ya kuleta mazingira rafiki na yenye ufanisi kati ya PDPC na DPOs.

“Tunatarajia kuanzisha mfumo wa mafunzo utakaoakisi uthibitisho wa kitaalamu wa DPOs. Hii inamaanisha kwamba, bila cheti rasmi cha utambuzi wako kutoka PDPC, huwezi kuwa DPO halali,” alisisitiza Dkt. Mkilia.

Hii ni hatua madhubuti inayolenga kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi, kuhakikisha maafisa wanaotekeleza majukumu haya wanazingatia viwango vya kitaifa na kimataifa, na kuleta ufanisi wa kiutendaji katika sekta hiyo muhimu kwa ulinzi wa faragha kwenye taarifa binafsi za watu na mashirika nchini.