PDPC YATANGAZA MAFUNZO KWA MAAFISA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

May 22, 2025, 3:50 p.m. PDPC YATANGAZA MAFUNZO KWA MAAFISA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) Mhandisi Stephen Wangwe leo Alhamisi tarehe 22/05/2025 ametangaza kuwepo kwa mafunzo maalum ya uzingatiaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi yatakayoanza rasmi mwezi Juni, 2025.

Akizungumza na waandishi habari katika ofisi za PDPC Dodoma, Mhandisi Wangwe amesema kuwa mafunzo haya yatawahusisha maafisa ulinzi wa taarifa binafsi (DPOs) na watumishi wengine ambao taasisi na kampuni zao zinapenda wapate ujuzi juu ya utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura namba 44 ya mwaka 2022.

“Mafunzo haya yanalenga kuwaelekeza maafisa ulinzi wa taarifa binafsi namna ya kulinda taarifa za taasisi na kampuni zao kwa kuhakikisha hazitumiki vibaya. Mafunzo haya pia yatasaidia kuongeza ustawi wa haki ya faragha na usalama wa watu hivyo Tanzania kuingia katika ulimwengu wa kistaarabu kupitia uhifadhi wa faragha za watu’’amesema Mhandisi Wangwe.

“Tume inazihimiza taasisi zote za umma na binafsi kuchangamkia fursa hii ya mafunzo ili utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi uwe na ufanisi nchini, ambapo tangazo rasmi la kujiandikisha kwa ajili ya mafunzo litatolewa kupitia tovuti ya tume www.pdpc.go.tz na vyombo mbalimbali vya habari” amesema Mhandisi Wangwe.

Mafunzo hayo yameandaliwa na PDPC na yatafanyika kwa mfumo wa makundi ya washiriki 400 kwa kila kundi ambapo washiriki watajengewa uwezo kuhakikisha taasisi zote nchini zinafikisha viwango vya kitaifa na kimataifa vya ulinzi wa taarifa binafsi.

Taasisi za umma na binafsi kujisajili PDPC ni takwa la kisheria na zoezi la usajili huo ni endelevu. Mpaka sasa jumla ya taasisi 9145 zimeshakamilisha usajili na wito umetolewa kwa taasisi zilizosalia kuhakikisha zinakamilisha usajili ili kuendana na matakwa ya Sheria.