PDPC Yatoa Mafunzo Maalumu kwa Bodi ya ERB Jijini Arusha

March 17, 2025, 9:23 p.m. PDPC Yatoa Mafunzo Maalumu kwa Bodi ya ERB Jijini Arusha

Leo Jumatatu tarehe 17/03/2025, Jijini Arusha, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imefanya mafunzo maalumu kwa Bodi na Menejimenti ya Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) katika hoteli ya Corridor Springs. Mafunzo hayo yamejumuisha mada mbalimbali zinazohusiana na ulinzi wa taarifa binafsi, yakilenga kuimarisha uelewa na utekelezaji wa sheria zinazohusiana na ulinzi wa taarifa kwa Bodi hiyo.

Mkurugenzi wa Usajili na Uzingatiaji wa PDPC, Mhandisi Stephen Wangwe, aliwasilisha mada kuhusu Chimbuko la Dhana ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, akielezea mchakato wa kuanzishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Namba 11 ya mwaka 2022 pamoja na kanuni zake. Alisisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi na jinsi ya kushughulikia malalamiko pamoja na haki za wahusika wa taarifa hizo.

Dkt. Noe Nnko, Mkurugenzi wa Tafiti za Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Teknolojia PDPC alitoa mada kuhusu teknolojia zinazoibuka na changamoto zinazohusiana nazo katika ulinzi wa taarifa binafsi. Dkt. Nnko pia alisisitiza ulazima wa ERB kuwa na maafisa ulinzi wa taarifa binafsi na mifumo thabiti ya kulinda taarifa binafsi za Wahandisi.

Aidha, Mkuu wa Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano wa PDPC, Bw. Innocent Mungy, alitoa mada kuhusu majukumu ya Tume, akieleza aina mbalimbali za taarifa zinazohitaji ulinzi, sababu za kuzilinda pamoja na madhara ya taarifa hizo kuvuja. Pia alizungumzia umuhimu wa kupata ridhaa za wenye taarifa kabla ya kutumia taarifa hizo na kufanya mabadiliko ya mitizamo kuhusu masuala ya faragha na ulinzi wa taarifa binafsi.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mhandisi Benard Kavishe, alitoa shukrani kwa PDPC kwa kutoa mafunzo hayo maalumu, akiongeza kuwa yatasaidia Bodi hiyo katika kutekeleza sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa ufanisi mkubwa.

Mafunzo haya ni moja ya hatua muhimu kwa PDPC katika kuhakikisha kuwa taasisi zinaweza kutimiza wajibu wao wa kulinda taarifa binafsi za wananchi, huku zikiimarisha uaminifu na usalama katika huduma zao na hasa katika uchumi wa kidijitali nchini.