ULINZI WA TAARIFA BINAFSI NI SWALA NYETI KATIKA MAENDELEO YA SAYANZI NA TEKNOLOJIA

March 29, 2025, 2:44 p.m. ULINZI WA TAARIFA BINAFSI NI SWALA NYETI KATIKA MAENDELEO YA SAYANZI NA TEKNOLOJIA

Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni suala nyeti kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia kunakosababisha utoaji huduma nyingi kuhamia kwenye mifumo ya kielektroniki hivyo kulazimu kuanzishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Namba 11 ya Mwaka 2022, Sura ya 44.

Hayo yameelezwa leo Machi 28, 2025 jijini Mwanza na Mkurugenzi  Mkuu wa PDPC, Dkt.Emmanuel Mkilia wakati akizungumza kwenye warsha ya dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi iliyoandaliwa na PDPC kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mwanza na Wadau wa Taasisi za umma na binafsi ambapo amesema maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani yameleta Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini.

“Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi inatoa muongozo wa kulinda haki na faragha kwa wananchi wote wa Tanzania kwa kuhakikisha  taarifa zao binafsi zinakusanywa na kuchakatwa kwa uwazi, usalama na kwa mujibu wa sheria”amesema Dk.Mkilia

Aidha Dkt. Mkilia amesema kuwa licha ya Mkoa wa Mwanza kuwa wa kimkakati hasa katika uchumi wa kidijitali, bado usajili wa Taasisi upo nyuma kutokana na kuwa mpaka sasa ni taasisi 20 pekee zilizosajiliwa kwenye mkoa huo.

“Taasisi zote za umma na binafsi zihakikishe zinajisajili PDPC kabla ya tarehe 30 Aprili 2025  na kuweka hatua madhubuti za kiusalama kulinda taarifa binafsi dhidi ya upotevu, ufichuaji usioidhinishwa au matumizi mabaya ya taarifa husika” amesema Dkt. Mkilia.

Akifunga warsha hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Hassan Masala amewataka viongozi wa taasisi za umma na binafsi zilizopo Mwanza kushirikiana na PDPC kuhakikisha usimamizi wa utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Sura ya 44 kwa maendeleo ya Taifa unazingatiwa.

“Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza hakikisha unashusha maelekezo haya katika Taasisi zilizopo chini yako ili utekelezaji ufanyike haraka iwezekanavyo sambamba na kuhakikisha taasisi zote zinateua Maofisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi (DPOs) ili kusimamia ulinzi wa taarifa hizo kwenye ofisi zao” amesema Mhe. Masala