‘UNWANTED WITNESS’ WATEMBELEA PDPC

Feb. 13, 2025, 10:29 p.m. ‘UNWANTED WITNESS’ WATEMBELEA PDPC

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) leo Februari 13, 2025 imepokea wageni kutoka kwenye asasi ya kiraia inayojulikana kwa jina la ‘Unwanted Witness’ iliyopo nchini Uganda. Asasi hii ya kiraia inalenga kukuza uhuru mtandaoni na kulinda haki za kidijitali nchini Uganda. Pia inalenga kuweka mazingira salama ya kidijitali kwa wananchi na kukuza matumizi sahihi ya teknolojia.

Akizungumza katika ofisi za PDPC zilizopo Njedegwa, Dodoma Bi. Freda Nalumansi Mugambe, kiongozi wa Utafiti na Utetezi wa asasi hiyo ameeleza kuwa wametembelea ofisi za PDPC kuomba ushirikiano katika uendeshaji wa kongamano la ulinzi wa faragha wanalotarajia kulifanya mwezi Septemba, 2025.

“PDPC ni wadau wakubwa kwenye ulinzi wa faradha, kwa mwaka huu kongamano la ulinzi wa faragha limeshirikisha nchi nne Uganda, Kenya, Tanzania na Rwanda ambapo awali lilihusisha Kenya na Uganda tu. Lengo la sisi kuja kwenu ni kuomba ushirikiano katika kuendesha mashindano ya kuwapata washindi kati ya wanafunzi wa sheria kutoka vyuo vikuu vya nchi washiriki ili kuwaongezea uelewa juu ya dhana ya faragha kwa kuwa wao ndiyo watakaosaidia upatikanaji wa haki  ya faragha katika utendaji kazi wao.”

Kwa upande wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Wakili Humphrey Mtuy, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PDPC Dkt. Emmanuel Mkilia, aliihakikishia asasi ya kiraia ya ‘Unwanted Witness’ kuwa PDPC itatoa ushirikiano kwao kwa kuwa jambo wanalolifanya linasaidia kuhakikisha faragha za watu zinalindwa hasa kupitia taarifa zao binafsi jambo ambalo ndilo kiini cha utendaji kazi wa PDPC.

“Yamekuwa mazungumzo mazuri baina ya PDPC na ‘Unwanted Witness’, PDPC tutawapa ushirikiano kwa kuwa jambo wanalolifanya linaendana na malengo yetu ya kutoa elimu kwa umma kuhusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi, na wanafunzi hao wa sheria wanaowalenga ni kundi muhimu kwetu kwa sababu ndio wanaotarajiwa kushughulika na maswala ya kisheria kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi.”

Kwa mwaka 2025, kongamano la ulinzi wa faragha litakuwa na kauli mbiu ‘Ulinzi wa taarifa na mfumo wa vitambulisho vya taifa’ (Data Protection and National Identification Systems) litakaloshirikisha wadau wa ulinzi wa taarifa wakiwemo wanafunzi wa sheria kutoka vyuo vikuu ambapo kwa Tanzania vyuo 19 vitashirikishwa kutafuta washindi watatu watakaopatiwa zawadi zikiwemo fedha taslimu na makombe, pia washindi hao watashiriki katika midahalo ya kitaaluma kuhusu ulinzi wa taarifa.