Sheria ya Ulinzi wa Taarifa binafsi ni mahusus kwa ajli ya kuweka masharti kuhusu misingi ya ulinzi wa Taarifa binafsi kwa lengo la kuweka kiwango cha chini cha matakwa ya ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi,kuanzisha Tume ya ulinzi wa Taarifa Binafsi, kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi.
Sheria ya Ulinzi wa taarifa binafsi ilianza kutekelezwa tarehe 01 Mei, 2023 ambapo matokeo ya utekelezaji wa Sheria hiyo ni uanzishwaji wa Tume ya Ulinzi Binafsi ambayo inamajukumu yafuatayo;
- Kusimamia utekelezaji wa Sheria;
- Kusajili wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi;
- Kupokea, kuchunguza na kushughulikia malalamiko kuhusu madai ya ukiukwaji wa ulinzi wa taarifa binafsi na faragha za watu;
- Kufanya tafiti na kufuatilia maendeleo ya Teknolojia kuhusiana na uchakataji wa taarifa; na
- Kuimarisha mashirikiano na nchi zingine.
Majukumu haya ya Tume yamezingatia misingi mikubwa ambayo nchi zote Duniani zinapaswa kuzingatia ili kuhakikisha taarifa binafsi za watu zinalindwa wakati wa ukusanyaji, uchakati, usambazaji na uhifadhi za taarifa binafsi, misingi hiyo ni;
- Ukusanyaji wa taarifa kihalali na kwa usawa
- Ukusanyaji wa taarifa lengo kusudiwa
- Ukusanyaji wa taarifa inayojitosheleza na iendane na lengo la Taasisi
- Ukusanyaji wa taarifa uwe sahihi na iwe ya wakati huo
- Ukusanyaji wa taarifa uhifadhiwe kwa muda muafaka kwa lengo husika
- Ukusanyaji wa taarifa ufanyike kwa kuzingatia haki zote za mhusika wa taarifa
- Mkusanyaji au mchakataji anawajibika kulinda taarifa binafsi
- Kuzingatia utaratibu wa usafirishaji wa taarifa nje ya mipaka ya Nchi
Tangu kuanzishwa kwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi masuala yafuatayo yametekelezwa;
BODI ya Wakurugenzi wa PDPC
Bodi ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa binafsi imeshaundwa tangu Disemba 2023. Bodi hiyo ina wajumbe saba (07) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mheshimiwa Balozi Adadi Mohammed Rajabu na Makamu Mwenyekiti wa Bodi Bi. Fatma Mohammed Ali ambao waliteuliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Kufuatia uteuzi wao, Waziri bwa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Moses Nnauye aliteua Wajumbe wengine ambao ni pamoja na Bwana Ramadhan Athumani mungi, Bwana Edward Samwel Lymo, Bwana Hamid Haji Machano, Bi Frida Peter Mwera na Bwana Maxcence Mello.
Kanuni za Ulinzi wa Taarifa Binafsi
Kanuni mbili (2) zimetungwa chini ya Sheria ya Ulinzi wa taarifa Binafsi Na. 11, 2022 ambazo ni:-
Kwanza, Kanuni za Ukusanyaji na Uchakataji wa Taarifa Binafsi za mwaka 2023 kupitia Gazeti la Serikali GN. 349 ya tarehe 12 Mei, 2023 Kanuni ya Ukusanyaji na Uchakataji wa Taarifa Binafsi inaainisha utaratibu wa usajili wa Wakusanyaji na Wachakataji wa Taarifa Binafsi; inaainisha utaratibu wa mhusika wa taarifa (data subject) kupata haki katika ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi zinazomhusu; utaratibu wa usafirishaji wa taarifa binafsi nje ya nchi; na inaweka wajibu kwa wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi hususan katika kuhakikisha uwekaji wa viwango vya usalama wakati wa ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi.
Pili, Kanuni za Taratibu za Kushughulikia Malalamiko ya Ukiukwaji wa Misingi ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi za mwaka 2023 kupitia GN. 350 ya tarehe 12 Mei, 2023. Kanuni za Taratibu za Kushughulikia Malalamiko ya Ukiukwaji wa Misingi ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi inaainisha taratibu za kuwasilisha malalamiko dhidi ya ukiukwaji wa misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi; taratibu za uchunguzi na usuluhishi wa lalamiko lililowasilishwa; na taratibu za kusikiliza malalamiko.
Miongozo ya Ulinzi wa taarifa Binafsi
Tayari miongozo minne (4) imeandaliwa, Mwongozo wa usajili wa wakusanyaji na wachakataji wa taarifa, Mwongozo wa kusimamia malalamiko, Mwongozo wa Sera ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na Mwongozo wa idhini ya mhusika wa taarifa.
Muundo wa Mgawanyo wa Majukumu
Muundo na Mgawanyo wa majukumu umekamilika na kuidhinishwa ambapo Tume itatekeleza majukumu yake Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwenye masuala yanayohusu mambo ya Muungano.
Ofisi ya Makao Makuu ya Tume
Ofisi ya Makao Makuu ya Tume kwa sasa ipo katika Jengo la Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF House) lililopo Njedengwa Jijini Dodoma na kuna Ofisi ya Tume Zanzibar iliyopo Ghorofa ya Nne (4) ya Jengo la Bombay Bazar Center Amani maeneo ya mzunguko wa Amani katika njia ya kuelekea Kwerekwe.
Hali kadhalika Tume imepata Kiwanja katika eneo la Njedengwa chenye ukubwa wa hektari 2.99 ambapo tayari maandalizi ya ujenzi wa ofisi za Tume yameanza ikiwemo maandalizi ya michoro.
Mfumo wa Kusajili Wakusanyaji na Wachakataji wa Taarifa Binafsi pamoja na Kushughulikia Malalamiko
Mfumo wa Kusajili Wakusanyaji na Wachakataji wa Taarifa Binafsi pamoja na Kushughulikia Malalamiko dhidi ya Ukiukwaji wa Misingi ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (RCMIS) umekamilika. Mfumo wa Kusajili Wakusanyaji na Wachakataji wa taarifa (RCMIS) una uwezo wa kufanya yafuatayo;
- Utambuzi na Usajili wa Wakusanyaji taarifa “Data Controller” na Wachakataji taarifa “Data Processor” na kutoa vyeti vya usajili. (Registration module);
- Usajili maafisa wa Tume wanaohusika na kushughulikia usajili ikiwa ni pamoja na msajili, mwidhinishaji pamoja na maafisa wote wa Tume wanaohusika na usajili, lakini pia usajili wa maafisa wawakilishi wa taasisi za Kukusanya na Kuchakata taarifa “Data Protection Officer”;
- Malipo kupitia mfumo wa kufanya malipo Serikalini “Government electronic Payment Gateway (GePG)”;
- Upokeaji na utoaji wa taarifa kwa umma (Notifications module);
- Utoaji Vibali kwa taarifa zinazovuka mipaka ya nchi (Permit module);
- Uwekaji na utoaji wa Ripoti ya kila robo ya mwaka kuhusu ulinzi wa taarifa kutoka kwa wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi (Reports module);
- Urekebishaji wa taarifa kutoka kwa wakusanyaji na wachakataji wa taarifa (Rectification module); na
- Kupokea malalamiko ya Mhusika wa taarifa “Data Subject”. (Complaints module).
Tume hii ni chombo muhimu katika maendeleo ya nchi kiuchumi hususan katika kipindi hiki ambapo dira ya nchi ni katika Uchumi wa Kidijitali ambapo taarifa imekuwa ni bidhaa muhimu, hivyo ili kufanikisha mageuzi ya uchumi wa kidijitali yanayozingatia faragha za watu, heshima zao na utu ili kujenga imani ya watumiaji wa huduma zinazotolewa kwa njia ya kidijitali pamoja na mifumo kusomana, matumizi ya jamii namba, mfumo wa utambuzi wa makazi na mfumo jumuishi wa malipo ni muhimu kulinda taarifa binafsin za watu na kujenga faragha kwao.
Tume hii ni chombo muhimu katika kuhakikisha maslahi ya uwekezaji wa ndani na nje ya nchi yanafanyika kwa tija na malengo kusudiwa pamoja na kuimarisha masuala ya kiusalama ya nchi.
WASILIANA NA TUME
TUSHIRIKIANE NA PDPC KUIMARISHA US…
Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi …
TOA TAARIFA ZAKO KULINGANA NA HUDU…
KILA TAASISI IWE NA SERA YA ULINZI…
JAMII X-CHANGE; UBUNIFU KATIKA MIF…
TUMIENI TEKNOLOJIA VIZURI KULINDA …
Mkutano wa Jumuiya ya Afrika Masha…
ULINZI WA TAARIFA BINAFSI UNAANZA …
PDPC KUSHIRIKIANA NA WADAU KUIMARI…
JAMII YASHAURIWA KULINDA TAARIFA B…
PDPC NA HILTON LAW GROUP WAKUTANA …
TUZINGATIE KANUNI ZA DHANA YA ULIN…