UTANGULIZI TUME YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini, ilianzishwa rasmi tarehe 01 Mei, 2023 kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Na. 11, 2022. Tume ilianza utekelezaji wa majukumu yake kama matokeo ya utekelezaji wa Sheria hiyo na kuanzishwa rasmi majukumu yake.

Tarehe 12 Septemba, 2021 kupitia Hati ya Mgawanyo wa Majukumu iliyotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na.782 la tarehe 22 Novemba, 2021 Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliundwa ambapo pamoja na majukumu mengine Wizara ilipewa jukumu la kusimamia Ulinzi na Usalama wa Mitandao nchini.

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni nyenzo mtambuka muhimu katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa hasa katika kipindi hiki cha Mapinduzi ya 4, 5 na 6 ya Viwanda. Pamoja na mafanikio yanayotokana na ukuaji wa TEHAMA duniani pia kumekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo ulinzi wa taarifa binafsi ambazo zimekuwa zikikusanywa, zikichakatwa na wakati mwingine kusafirishwa kutoka nchi moja kwenda nyingine bila kuzingatia utaratibu na misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi iliyokubalika duniani.

Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya mbalimbali za Kikanda na Kimataifa zikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU). Kwa kuwa suala la mitandao halitambui mipaka ya kijiografia, nchi wanachama wa Jumuiya hizo zimekubaliana kuwa na Sheria mahususi na Taasisi Huru katika kukabiliana na changamoto hizo.

Jumuiya ya Afrika Mashariki iliandaa Mwongozo wa Sheria za Usalama wa Mtandao mwaka 2008; Jumuiya ya SADC iliandaa Sheria tatu za mfano za Usalama Mtandao za mwaka 2012; na Umoja wa Afrika iliandaa Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Usalama Mtandao na Ulinzi wa Taarifa Binafsi pia maarufu kama Mkataba wa Malabo wa mwaka 2014 ambapo Mikataba na Miongozo hiyo kwa pamoja inazitaka nchi wanachama kuwa na Sheria tatu za msingi za usalama wa mtandao na Taasisi huru, Sheria hizo ni Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ambayo itaanzisha Tume huru ya kusimamia ulinzi wa taarifa binafsi. Pia, nchi za Ulaya nazo zimeandaa Mwongozo wa kukabiliana na changamoto hizo.

Takwimu zinaonyesha kuwa nchi mbalimbali zimetunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kama ambavyo imebainishwa. Nchi 162 kati ya nchi 198 Duniani zimetunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Nchi 36 kati ya nchi 54 za Afrika tayari zimetunga Sheria hiyo. Nchi 12 kati ya nchi 16 za SADC zimeshatunga Sheria hiyo. Nchi 4 kati ya nchi 6 za EAC zimetunga Sheria hiyo. Nchi ya Burundi na Sudani ya Kusini ziko kwenye mchakato wa kutunga sheria hii.

Tanzania imekamilisha uandaaji wa Sheria hizo tatu za msingi ambazo ni Sheria za Makosa ya Mtandao 2015, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, 2015 na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa ya mwaka 2022. Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Na.11 ya mwaka 2022 ni Sheria muhimu kwa Taifa letu kwani ni Sheria ambayo inaweka utaratibu wa kulinda haki ya faragha ya Mtu kama ambavyo imebainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ibara ya 16 (1)(2) na Ibara ya 15 ya Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo katiba zote mbili zinazungumzia  haki ya faragha na usalama wa mtu "Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, Maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake, pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake binafsi".

Pia Ibara hizo, zimeainisha wajibu wa Serikali ambapo imeelezwa kuwa "kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kwa mujibu wa Katiba, Mamlaka itaweka  utaratibu wa sharia kuhusu hali, namna na kiasi ambacho haki ya mtu na faragha na usalama wa nafsi yake, mali yake na maskani yake yanaweza kuingiliwa bila kuathiri ibara hii"”.

Kuwepo kwa Sheria hii, ni utekelezaji matakwa ya Katiba na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Ibara ya 61(b) ambayo imeelekeza kuongeza ufanisi na usiri wa Taarifa za wananchi katika mawasiliano kwa kutunga Sheria ya kuimarisha ulinzi wa taarifa na takwimu.

....READ MORE