Mkurugenzi Mkuu

Emmanuel Mkilia

Mkurugenzi Mkuu

Karibu kwenye Tovuti ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania!

Tunakushukuru na tunatoa salamu za furaha na shukrani kwa kutembelea tovuti yetu.

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi inajivunia kuwa mwongozo wa kipekee katika kulinda haki zako za faragha nchini Tanzania. Kama mwanachama wa Jumuiya za Kikanda na Kimataifa, Tanzania inatambua umuhimu wa kuwa na sheria na taasisi huru za kukabiliana na changamoto za ulinzi wa taarifa binafsi. Lengo letu ni kuwezesha matumizi salama ya taarifa binafsi na yanayozingatia Sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa.

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania, tunatilia maanani misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, na Umoja wa Afrika na Jumuia ya Kimataifa kwa ujumla katika kuanzisha Sheria muhimu za Usalama wa Mtandao. Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 inasimamia haki yako ya faragha kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyoelekeza utekelezaji wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini.

Tume yetu, iliyoanzishwa mnamo Mei 2023, ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Na. 11 ya mwaka 2022. Tunasajili wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi, tunapokea malalamiko ya ukiukwaji wa faragha na ulinzi wa taarifa binafsi na kuyatatua, tunafanya utafiti, na kushirikiana na nchi zingine katika suala zina la Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Pamoja na kanuni zetu za ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi, tunahakikisha ulinzi wa taarifa unaendana na viwango vya kimataifa kama inavyotarajiwa.

Tume ina mfumo wa kisasa wa kusajili wakusanyaji na wachakataji wa taarifa, pamoja na mfumo wa kushughulikia malalamiko, ili kuhakikisha utaratibu mzuri wa utoaji na usimamizi wa taarifa unafuatwa kwa mujibu wa Sheria. Jukumu letu ni kuhakikisha tunaweka misingi ya kuwezesha matumizi salama ya Taarifa Binafsi nchini Tanzania. Tovuti hii itakuwa inatoa taarifa kuhusu Tume kwa ujumla, taarifa za maaumuzi ya Bodi ya Tume, utekelezaji wa usimamizi wa kanuni zinavyotekelezwa na kutoa taarifa za miongozo ya ulinzi wa taarifa binafsi.

Tunatambua umuhimu wa teknolojia na mabadiliko ya kidijitali katika maendeleo ya nchi yetu. Hivyo, tunazingatia utekelezaji wa kuzingatiwa kwa haki za faragha na usalama wako wakati wa kukusanya, kuchakata, kusambaza, na kuhifadhi taarifa zako binafsi. Tunakukaribisha kufuatilia kwa karibu maendeleo yetu na kutumia huduma zetu kwa imani na uhakika wa ulinzi wa taarifa zako binafsi.

Tafadhali jisikie huru kuwasiliana nasi kwa maelezo zaidi au kutoa maoni kupitia anwani zetu kama ilivyobainishwa na pia kwa kutumia akaunti zetu za mitandao ya kijamii. Asante kwa kuwa nasi katika safari hii ya ulinzi wa faragha na taarifa binafsi kama mdau wetu!

Asante kwa ushirikiano wako.

Tazama Wasifu

Faragha Yako ni Wajibu Wetu.

Emmanuel Mkilia

Mkurugenzi Mkuu

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania